Advertisements

Wednesday, December 7, 2016

WAZIRI MKUU AAGIZA UONGOZI WA NCAA KUMPELEKEA NYARAKA ZA FARU JOHN IFIKAPO DESEMBA 8, 2016

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameugiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kumpelekea nyaraka zote zilizotumika katika kumuhamisha faru maarufu kwa jina la John katika hifadhi hiyo ifikapo Desemba 8, 2016.

Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Desemba 6, 2016) alipotembelea Ofisi za makao makuu ya NCAA, zilizoko wilayani Ngorongoro mkoa Arusha wakati akizungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani hapa.

"Nina taarifa zenu kuwa mlimuhamisha kwa siri faru John kreta na kumpeleka V I P Grumet Serengeti Disemba 17, 2015 na mliahidiwa kupewa sh. milioni 200 ambapo mkapewa sh. milioni 100 kwa ahadi ya kumaliziwa sh. milioni 100 nyingine baadaye,".

“Naomba niletewe nyaraka zote zilizotumika kumuomba na kumuondoa faru huyo na barua zilizotumika kujadili suala la faru John. Nasikia amekufa naomba pembe ziletwe ofisini na iwapo itathibitika aliondoka bila ya kufuata taratibu wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria,”.


Katika hatua nyingine Waziri Mkuu apega marufuku tabia ya baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo ambao wanawakabidhi watoto kupeleka ng’ombe wao ndani ya kreta. “ Watumishi wa Ngorongoro ndiyo wanaopeleka ng’ombe ndani ya kreta na si wenyeji. Sasa marufuku na tutakayemkuta hatutakuwa na msamaha naye,”.

Amewataka watumishi hao kuhakikisha wanakuwa waadilifu na wanafanyakazi kwa kufuata misingi ya kiutumishi na kuacha tabia za kuendekeza rushwa na wizi.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa NCAA, Sezzary Simfukwe kutokana na tuhuma za ubadhilifu wa fedha zinazomkabili na tayari anahojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

"Haiwezekani mtumishi awe anachunguzwa na TAKUKURU halafu aendelee kuwa ofisini si atavuruga uchunguzi. Asimamishwe kazi kuanzia leo mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika na aikibainika kwamba hana hatia atarudi kazini,” alisema.

Pia Waziri Mkuu alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa NCAA, Fred Manongi kueleza zilipo sh. bilioni moja zilizotolewa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete kwa ajili ya kujengea ranchi ya wafugaji wa tarafa ya Ngorongoro.

Akijibu swali hilo Manongi alisema wakati Rais Kikwete anatoa fedha hizo alikuwa bado hajateuliwa kushika washifa huo, ambapo Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi huyo kufanya uchunguzi juu ya fedha hizo na kasha kumpelekea tarifa.
 

IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU

1 comment:

Anonymous said...

Kuna shida somewhere, yaani hata swala hili ni mpaka Prime minister a intervene? Hawa watendaji wengine wako wapi? hao wote waliifahamu issue hii na kuikalia kimywa wanapaswa kuwajibika pia.