Advertisements

Wednesday, January 18, 2017

TANZANIA KUANZA KUTUMIA MFUMO WA DIRISHA MOJA LA HUDUMA (ELECTRONIC SINGLE WINDOW SYSTEM)

Kaimu Kamishna Mkuu TRA, Mary Maganga.

Katika kuhakikisha inaboresha huduma kwa wafanyabiashara ambao wanaingiza mizigo nchini kwa njia ya bandari, mipaka na viwanja vya ndege, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imeeleza mpango wa Serikali wa kuanza kutumia mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (Electronic Single Window System) ambao kwa hakika utamaliza tatizo la mizigo kukaa muda mrefu kwa sababu ya kukosekana vibali. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika mafunzo ya siku moja kuhusu mfumo wa Dirisha Moja la Huduma kwa taasisi zinazotoa vibali na wafanyabiashara, Meneja Mfumo wa Kieletroniki wa Dirisha Moja la Huduma, Tinka Felix alisema lengo la kuanza kutumia mfumo huo ni kuboresha huduma ambazo wanazitumia sasa ili wafanyabiashara wanaoingiza mizigo nchini waweze kuipata kwa haraka kuliko ilivyo sasa.
Meneja Mfumo wa Kieletroniki wa Dirisha Moja la Huduma, Tinka Felix akizungumza kuhusu mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (Electronic Single Window System). (Picha zote na Rabi Hume - MO DEWJI BLOG)

“Ni mpango wa Serikali kuboresha huduma kwa wateja kwa kupunguza muda wa kutoa mizigo bandarini au mipakani au kwenye viwanja vya ndege, kupitia mfumo huu wateja hawatakuwa wakienda kwenye idara na taasisi za Serikali na badala yake wakiwa hukohuko kwenye ofisi zao wataweza kuomba na kupata vibali na kupata bili za malizo kwenda kulipa benki, mfumo pia utafanya kazi na benki," alisema Felix. Alisema Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kutumia mfumo huo na mataifa mengi yanautumia ili kurahisisha huduma kutolewa kwa haraka kwani mfumo wa sasa wa forodha (tancis system) unashindwa kufanya kazi kwa haraka jambo ambalo linasababisha mizigo kuchelewa kutolewa kutokana na muda mrefu mmiliki kutumia kutafuta vibali.
Mkurugenzi wa Sera Utafiti Na Ushauri wa TPSF, Gili Teri akizungumza faida za kutumia mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (Electronic Single Window System).

“Mfumo wa sasa ili mtu apate kibali anatakiwa atembelee hizo ofisi hata mara 10 na baadhi ya ofisi wanataka vibali zaidi ya kimoja lakini mfumo huu wa sasa muda ambao unatumika kuomba vibali utapungua na tunategemea kuokoa Dola milioni 65 kwa kutumia tu mfumo wa electronic single window system,” alisema Felix. Alisema kwa sasa kuna taasisi za Serikali 47 ambazo zinatoa vibali lakini mfumo wa Dirisha Moja la Huduma utatumiwa na taasisi 32 ambazo kwa pamoja zitakuwa zikitoa vibali 106. Aidha alisema Serikali imeagiza kuwa mfumo huo uanze kutumika baada ya mwaka mmoja hivyo wanategemea kuanzia mwakani mfumo ambao watakuwa wakitumia utakuwa ni wa Dirisha Moja la Huduma (Electronic Single Window System) ambao utawezesha wafanyabiashara ambao wanatoa mizigo kupitia bandari, mipaka au viwanja vya ndege kupata vibali kwa haraka. Na Rabi Hume, MO DEWJI BLOG
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo ya siku moja wakiuliza maswali na kutoa maoni kuhusu mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (Electronic Single Window System).

No comments: