Advertisements

Wednesday, February 22, 2017

BARABARA YA MTWARA-MASASI KM 210 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,  Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Nnivata kilichopo mkoani Mtwara kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Mtwara-Masasi yenye urefu wa KM 210 itakayojengwa kwa kiwango cha lami wakati alipokuwa akiikagua barabara hiyo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wananchi wa Nanyamba katika mkutano wa hadhara kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Mtwara-Masasi yenye urefu wa KM 210 itakayojengwa kwa kiwango cha lami wakati alipokuwa akiikagua barabara hiyo, mkoani Mtwara.
 Muonekano wa sehemu ya kwanza ya barabara ya Mtwara-Nnivata yenye urefu wa KM 50 itakayoanza kujengwa mwezi Aprili mwaka huu kwa kiwango cha lami. Mradi huo utagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 89.5
 Muonekano wa Korongo lililoko kwenye moja ya barabara za Newala Mjini ambalo limetokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Mtwara.
Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini Mhe. George Mkuchika (wa pili kulia), akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), eneo lililoathiriwa na mvua (halipo pichani), zinazoendelea kunyesha katika moja ya barabara jimboni hapo mkoani Mtwara.  Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo.


Serikali imesema itaanza ujenzi wa barabara ya Mtwara-Masasi KM 210 sehemu ya Mtwara-Nnivata yenye urefu wa KM 50 kwa kiwango cha lami mwezi Aprili mwaka huu, ili kurahisisha usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo na kufungua fursa za kiuchumi katika mkoa huo na nchini jirani ya Msumbiji.
Akizungumza na wananchi wa Nanyamba wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa mkandarasi Dott Services Ltd ataijenga barabara hiyo kwa viwango vya kisasa na kwa gharama za shilingi bilioni 89.5.
"Mkandarasi atafika eneo la mradi mwezi wa nne mwaka huu na ujenzi utaanza mara moja, hivyo wananchi muwe na subira ili muweze kunufaika na barabara hiyo pindi itakapokamilika kwa kuwa itazidi kuchochea maendeleo yenu na Taifa kwa ujumla", amesema Waziri Mbarawa.
Waziri Profesa Mbarawa amefafanua kuwa ujenzi huo utadumu kwa miaka miwili tangu kuanza kwa ujenzi wake hadi kukamilika, hivyo Prof. Mbarawa amewataka wananchi wa Mtwara kutoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Aidha, Waziri Mbarawa ameongeza kuwa kwa wale wananchi waliovunjiwa nyumba zao na kustahili kulipwa fidia kisheria ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo watalipwa, na kazi ya kutathimini nyumba hizo itaanza mapema mwezi wa tatu mwaka huu.
Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itaongeza fedha za ujenzi wa barabara hiyo kwa awamu nyingine katika Mwaka wa fedha 2017/2018 ili kuweza kufungua barabara yote kwa kipindi kifupi.
Kuhusu huduma za mtandao wa mawasiliano mkoani humo Prof. Mbarawa amewahakikishia wananchi kuleta huduma hiyo katika wilaya zote kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ili kurahisisha mawasiliano ambapo kwa sasa hali ya huduma ya mawasiliano katika baadhi ya vijiji hairidhishi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw. Evod Mmanda amesema kuwa barabara hiyo ikikamilika itarahisisha usafiri wa abiria na mizigo ikiwemo mazao yanayolimwa katika mkoa huo hususan zao la Korosho ambalo ni miongoni mwa mazao yanayoongeza pato kubwa kwa Taifa.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Mtwara-Tandahimba-Newala-Masasi yenye urefu wa KM 210 ambao unatarajiwa kuanza mwezi Aprili mwaka huu unatarajiwa kuunganisha wilaya tano za mkoa wa Mtwara na hivyo kufungua fursa za kiuchumi na kijamii katika Mkoa huo na nchi jirani ya Msumbiji.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments: