Advertisements

Wednesday, August 16, 2017

NI DIASPORA GANI SERIKALI YA MAGUFULI INAWATAKA NA KUWAPENDA

Na. M. M. Mwanakijiji

Mojawapo ya hoja ninazozisikia mara nyingi tangu Rais Magufuli achaguliwe kuwa Rais mwaka 2015 ni kuwa hapendi Watanzania walio nchi za nje na kuwa ana uhasama wa wazi na Watanzania wanaoishi na kufanya kazi nchi za nje. Kwamba, yeye au watu wake wa karibu wanaona kuwa Watanzania hawa wanataka “kote kote”; kwamba wanataka kuishi na kufanikiwa nchi za nje na wakati huo huo wanataka wachukuliwe kama Watanzania wengine wakiwa na haki zote.

Mara kwa mara viongozi wa Serikali (kuanzia Rais hadi wabunge) wanapoenda nje ya nchi hufanya jitihada ya kukutana na “Watanzania” wanaoishi nchi hizo. Huu si utaratibu mgeni na umekuwepo kwa muda mrefu. Mara kwa mara tunaona picha za viongozi hao wakikutana na kuzungumza na Watanzania hao na kusikiliza maswali yao mbalimbali na kujibu hoja zao mbalimbali. Kundi hili la Watanzania wanaoishi nchi za nje wanaitwa kama “diaspora”.

Neno hili “diaspora” lina asili ya neno la Kigiriki la “diaspeirein” lenye maana ya “kutawanya, kusambaza”. Neno hili kwa maana yake ya kwanza kabisa lilikuwa linatumiwa kuelezea Wayahudi waliotawanyika nje ya Israeli kufuatia uhamisho wa Babeli. Miaka ya karibuni hivi neno hili limekuwa likitumiwa kuelezea watu wote au jamii ya watu ambao wametawanyika sehemu mbalimbali nje ya nchi zao za asili. Hivyo, watu weusi waliotawanyika nje ya Bara la Afrika wanaweza kuitwa “diaspora” na Wahindi waliotawanyika nje ya India wanaweza kuelezewa hivyo hivyo.

Hata hivyo, neno hili lilipotumiwa kwa Wahayudi lilikuwa hasa linamaanisha watu waliopelekwa uhamishoni, waliolazimishwa kutoka katika nchi yao na kutawanyika duniani. Wayahudi hawa hawakuondoka Palestina ya kale kwa hiari yao bali waliondoka kwa kulazimishwa wakati mababu zao walipochukuliwa utumwa Babeli. Kwa Waafrika mfano sahihi wa watu walio kwenye dayaspora ni wale wote waliochukuliwa utumwa na uzao wao. Kwa muda mrefu wale wahamiaji wengine ambao wanaenda nje kwa hiari na kuamua kuishi huko kwa hiari walikuwa wanajulikana kama ‘wahamiaji” au “wahamiaji wa kigeni” (alien immigrants). Wahamiaji hawa wengi bado wana mawasiliano na mahusiano na nchi zao za asili.

Hata hivyo, sasa hivi neno hili ‘diaspora’ linajumuisha makundi yote mawili; yale yanayotokana na masalia ya utumwa (kama Wamarekani Weusi) na wale wahamiaji weusi. Hata hivyo, katika kundi hili la pili tunaweza kuligawa katika makundi mengine mawili – kundi la wahamiaji ambao bado wana uraia wa Tanzania na wahamiaji ambao wamechukua Uraia wa nchi hizo nyingine na hivyo hawana uraia wa Tanzania tena.

Hapa ndipo msingi wa swali langu upo; je serikali yetu inataka kuhusiana na ‘diaspora’ wapi hasa? Je, ni wale ambao wako katika nchi za kigeni lakini bado wana uraia wa Tanzania tu au inajumuisha na wale ambao wana asili ya Tanzania lakini wameshachukua uraia wa kigeni?

Jibu la swali hili ni rahisi; kwa kuangalia serikali inavyoshughulika na makundi haya mawili ni wazi kuwa Serikali haina sera, utaratibu au mfumo wowote unaowatambua kwa namna, njia, mpango, utaratibu au mwelekeo wowote wa kufuatilia mambo yanayowahusu Watanzania walioacha uraia wa Tanzania na kuwa raia wa nchi nyingine.

Mwaka jana Waziri wa Ardhi William Lukuvi (pichani) akitekeleza maamuzi na msimako wa Serikali ya Rais Magufuli alitangaza umma kuwa Watanzania diaspora (walio na uraia wa nchi nyingine) hawastahili kumiliki ardhi Tanzania hata kama ardhi hizo walizipata wakiwa Watanzania (kabla ya kuchukua uraia wa nchi nyingine). Lukuvi alinukuliwa kusema “Mtu akishaukana uraia wa Tanzania hana haki tena kama raia wa Tanzania, hivyo atamiliki ardhi kama mwekezaji na siyo raia, ardhi itabaki kuwa ya Watanzania tu, tutawasaka wale wote ambao wanamiliki ardhi kinyume na sheria za nchi”.

Kuna Kongamano linapangwa kufanyika huko Zanzibar ambalo linawahusu “Diaspora” (Watanzania wanaoishi nje ya nchi) Augusti 23, 24. Ni wazi kuwa wanaowataka siyo watu wenye asili ya Tanzania ambao wanaishi nje ya nchi, bali wale Watanzania (wenye uraia wa Tanzania bado). Kama hili ni kweli, ni muhimu sana kwa Serikali kuwa muwazi – waseme wanaowataka ni WALE WENYE URAIA WA TANZANIA TU. Kwa sababu kwa wale wengine ambao wana asili ya Tanzania, hata kama wana familia, ndugu, jamaa huko lakini wana uraia wa nje, hawa SIYO WENZETU ( kwa msimamo wa serikali).

Lakini pia watu wenye asili ya Tanzania ambao wana uraia wa nchi nyingine, hata kama wanamapenzi kiasi gani na Tanzania ni wakati na wao waanze kufikiria maslahi yao zaidi na ya watoto wao. Kwanini watu hawa wanajitahidi kusaidia nchi ambayo “siyo yao” na wanajitahidi kupeleka misaada huko wakati serikali ina uhasama nao? Sina tatizo mtu akiamua kumtumia hela kidogo ndugu yake au ndugu zake kuwasaidia maana hiyo ni damu yake, lakini kwanini mtu ahangaike na mambo mengine wakati angeweza kufanya mambo hayo Uganda, Congo, Kenya au Uganda au nchi nyingine yeyote? Kwanini mtu mwenye asili ya Tanzania atake kuwekeza Tanzania wakati angeweza kuwekeza nchi nyingine ambapo angeweza kupata faida zaidi na labda biashara yake ingekuwa na usalama zaidi?

Jambo hili limeanza kuwa na matokeo; nimeshakutana na baadhi ya ndugu zetu wenye asili ya Tanzania ambao wameanza kuachana na mawazo ya kuwekeza nyumbani na badala yake wanafikiria kuwekeza na kujiwekeza zaidi katika nchi zao hizi mpya. Hili si jambo geni kwani jamii nyingine za kigeni (kama hapa Marekani) zimejijenga katika nchi hii na kuzidi kufanikiwa.

Lakini jambo hili linaendana pia na mfumo wa serikali ambapo imejenga utaratibu wa kumvua mtu uraia wa nchi yake hata kama mtu huyo hajaukana uraia huo kwa hiari yake. Lukuvi alisema “mtu akishaukana uraia”; ukweli ni kuwa wengi wa ndugu zetu hawa hawajaukana uraia wao; wamenyang’anywa uraia huo kibabe. Mtu anapoukana uraia anaukana kwa sababu fulani na anaulizwa kuwa anaukana uraia huo; mfumo wetu umetengeneza utaratibu tu kuwa mtu anaukana uraia kwa sababu tu amechukua uraia wa nchi nyingine. Marekani kwa mfano, haijali kabisa mtu anauchukua uraia wa nchi gani, kwa kadiri ya kwamba hajasimama mahakamani kuukana uraia wa Marekani basi Marekani inautambua uraia wake kwanza. Kama mtu hajaamua kuukana uraia wa Tanzania kwanini Tanzania imnyang’anye uraia wake hasa kama bado ana mapenzi na utii kwa Tanzania?

Nitalizungumzia hili wakati mwingine lakini itoshe kusema tu kuwa Serikali inahitaji kukaa chini na kuja na sera yenye mantiki inayohusiana na watoto wa Watanzania waliotawanyika pote duniani. Ni maslahi na ni jema zaidi kuendelea kuwa na ushirikiano rasmi na watoto hao hata kama wamechukua uraia wa nchi nyingine. Hii haina maana mtu hawezi kuukana uraia wa Tanzania. Lakini tuweke utaratibu ambapo unampa mtu haki hiyo bila kumlamisha mwingine kupoteza uraia wa Tanzania. Uraia wa Tanzania usifutwe au kuondolewa isipokuwa kwa mtu kwa hiari yake kukana mahakamani. Usiondolewe kwa ndoa au kwa mtu kuchukua uraia wa nchi nyingine. Tuutukuze uraia wetu na kuufanya uwe vigumu kuufuta.

Lakini kama serikali imeamua kuendelea na mfumo huu kandamizi na kama bado imeamua kuona kuwa Watanzania walio na uraia wa nchi nyingine si “Watanzania tena” basi kuanzia sasa serikali inapopanga masuala ya kuzungumza na “diaspora” iweke wazi na bayana kuwa inataka kukutana na WALE TU ambao hawana uraia wa nchi nyingine. Viongozi wanapokuja nje na wanataka kukutana na watu wenye asili ya Tanzania waseme mapema kuwa wanataka kukutana na watu wenye uraia wa Tanzania na wahakikishe kuwa wanaokuja wanaangalia paspoti zao ili wageni (hata kama wana asili ya Tanzania) wasiingie kwenye mikutano hiyo. Kama hawawezi kumiliki ardhi kwa sababu ni wageni, mawazo yao ya nini?

Lakini pia nina wito wa uchokozi; jumuiya za Watanzania zilizoko nje ya nchi japo wenyewe kwa wenyewe hatuulizani nani ni “raia na nani si raia” wakati umefika na sisi tulio katika diaspora kuwa na msimamo wa pamoja; viongozi wanapokuja na kutaka kukutana nasi tuwaulize kama wanataka kukutana na wale wenye uraia wa Tanzania tu au hata wasio na uraia huo hata kama ni wenye asili ya Tanzania? Wakisema “wenye uraia tu” TUSIKUBALI KUKUTANA NAO. Tukikubali tutakuwa tumekubali wao watutenganishe!

Diaspora ni watu wamoja, ni wakati sasa wa kuonesha umoja na nguvu yetu kama wamoja hadi pale Serikali itapokuja na sera yenye mantiki ambayo itaheshimu utu wetu kama Watanzania na watu wenye asili ya Tanzania. India kwa mfano, inautaratibu wa “Raia wa India walio Ng’ambo” yaani Oversea Citizens of India (OCI). Huu ni utaratibu wao walioubuni kwani India kama Tanzania hairuhusu Uraia wa nchi mbili.

Lakini je sisi kama taifa tumeshindwa kubuni kitu chetu wenyewe na kuhakikisha kuwa jamii yetu walioko nyumbani, waliko kwenye jirani za Kiafrika na walio katika nchi za mbali nao wanaheshimiwa na kuthaminiwa kama raia wengine wa Tanzania?

Au tuulize tena ni ‘diaspora’ gani ambao Serikali inawataka na kuwajali na iko tayari kufanya nao kazi kwa manufaa ya Tanzania? Binafsi ni muumini wa Uraia wa Tanzania Kwanza. Ni muumini wa dhana ya uraia ya Mwalimu Nyerere ambayo uraia msingi wake ni utii kwa nchi yetu. Kama mtu hajaondoa utii na mapenzi kwa Tanzania hakuna sababu ya msingi ya kumnyang’anya uraia wake kama vile tulimpa kama zawadi wakati alizaliwa nao!

No comments: