Advertisements

Tuesday, August 15, 2017

Wapiga Debe Waanza Kuondolewa Rasmi Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeanza kutekeleza operesheni iliyoitangaza wiki iliyopita kwa kuwaondoa wapigadebe kwenye vituo vya daladala kutokana na kuwa chanzo cha wizi.

Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Lucas Mkondya,  jana alisema kuwa, operesheni hiyo imeanza jijini baada ya kukithiri kwa kesi zitokanazo na wizi kwenye vituo hivyo.

Alisema kwa siku kunaripotiwa matukio 20 hadi 50 ya wizi kwenye vituo vya daladala jijini huku wapigadebe wakidaiwa kuwa kichaka cha wizi huo.

Alisema operesheni hiyo, itakayoendeshwa kwa wiki nzima imelenga kuvifanya vituo hivyo kuwa maeneo salama.

“Vituoni kunakuwa na wizi na wezi wanafahamika, sasa ni mkakati wa kuwaondoa na kama wiki ikimalizika wizi haujaisha, tutawaondoa wote ambao hawana shughuli maalum vituoni hata kama hawapigi debe,” alisema.


Agizo la Kamanda Mkondya si jipya hata hivyo kwa wapiga debe baada ya maazimio kama hayo, kadhaa kushindwa katika miaka ya nyuma.

Akizungumza Machi 16, mwaka jana jijini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawane alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha anawaondoa wapiga debe wote kwenye vituo vya mabasi kwa sababu hizo hizo.

Waziri Simbachawene alitoa agizo hilo, wakati wa semina kwa wakuu wa mikoa wote nchini ambao walikuwa wameapishwa na Rais John Magufuli, Ikulu katika siku iliyotangulia.

Waziri huyo, alisema kazi ya kupiga debe sio rasmi na isiyo na kipato kitachoweza kumkwamua kijana husika kuondokana na umaskini.

“Namuomba Mkuu wa Mkoa ahakikishe anawaondoa hawa wapiga debe kwenye vituo vya mabasi kwa kuwa wamekuwa wakichangia kutokea kwa uhalifu," alisema Simbachawene.

"Kipato cha mpiga debe kwa siku hakiwezi kumkwamua kimaisha, sana sana wanatumia nafasi hiyo, kufanya uhalifu.
Wanatakiwa kuondolewa haraka waende kwenye kazi hata za kilimo.”

No comments: