Advertisements

Monday, October 23, 2017

Rais Magufuli amteua Profesa Luoga kuwa Gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BOT)

Rais John Magufuli amemteua Profesa Florens Luoga kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) kuchukua nafasi ya Profesa Benno Ndullu anayemaliza muda wake.
Rais Magufuli amesema hayo leo Jumatatu akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kutoa vyeti kwa kamati zilizohusika na ripoti za madini nchini.
Ndullu, ambaye amekuwa Gavana wa BOT tangu 2008 anamaliza muda wake Januari mwakani, miezi mitatu ijayo.
Akizungumza baada ya kutoa vyeti hivyo amesema kuwa atamteua gavana kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa kamati ya mashauriano kuhusu madini kutokana na kuridhishwa na kazi yao.
Hata hivyo aliamua kumtaja Profesa Luoga kuwa ndiye atakuwa Gavana mpya wa BoT.
Rais Magufuli amesema anajua kuwa hakumwambia, lakini tayari amemteua Profesa Luoga.
Huo ni uteuzi wa pili kwa Profesa Luoga, kwani Julai 11 mwaka huu Rais Magufuli alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA).
Profesa Luoga alichukua nafasi ya Bernard Mchomvu ambaye bodi yake ilivunjwa na uteuzi wake kutenguliwa.

No comments: