Advertisements

Monday, October 23, 2017

WAUMINI KKKT SIKONGE WAPONGEZA UTENDAJI WA RAIS MAGUFULI, WAMWOMBEA

Na Mussa Mbeho , Sikonge

WAUMINI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Sikonge Mkoani Tabora wamefanya Ibada Maalumu ya kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli na kupongeza utendaji wake.

Pongezi hizo zimetolewa jana katika Tamasha Maalumu la maombi na uzinduzi wa albamu ya Mchungaji Egon Israel lililoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Sikonge Peresi Magiri.

Mchungaji wa Kanisa hilo Yeremia Kiula Kitila alisema amani iliyopo hapa nchini na kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Rais John Pombe Magufuli ni ishara tosha kwamba Mungu anasikia maombi ya Watanzania na ataendelea kufanya makubwa kupitia Rais wetu.

‘Tunampongeza sana Rais kwa jitihada zake nzuri za kulinda, kutetea na kupigania rasilimali za nchi hii ili ziwanufaishe Watanzania wote’, alisema.

Aliongeza kuwa wataendelea kumwomba Mungu ili aendelee kumpa afya njema, ujasiri na hekima yeye na wasaidizi wake wote ili waweze kusimamia vyema rasilimali za nchi hii na kuwa chachu ya maendeleo ya wananchi.

Mchungaji Egon Israel wa kanisa la Pentekoste Victorious la mjini Tabora aliyekuwa akizindua albamu yake ya nyimbo za injili wilayani humo alisema Rais Magufuli hataki makuu, dhamira yake ni moja tu kuleta maendeleo na kuhakikisha rasilimali zilizopo hapa nchini
zinawanufaisha wananchi wote.

Mkuu wa wilaya hiyo Peresi Magiri aliungana na mamia ya waumini wa kanisa hilo kumwombea Rais ili kasi ya Utendaji wake iendelee hivyo hivyo kwa manufaa ya wananchi na MUngu awape weledi viongozi wote wa Serikali ya awamu ya tano.

Aliwataka Watumishi wa Mungu na waumini wote wa madhehebu ya dini kuendelea kumwombea Rais na wasaidizi wake wote ili kufanikisha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Peter Nzalalila alisema maombi ni muhimu sana kwa kuwa yatasaidia kumpa afya njema Rais wetu na wasaidizi wake wote na kumwongezea hekima na ujasiri wa kusimamia maendeleo ya nchi hii.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Simon Ngatunga alimpongeza Rais kwa kudhibiti mianya ya rushwa, wizi wa rasilimali za nchi ikiwemo madini huku akibainisha kuwa maombi hayo yatamwongezea Rais ari, nguvu na kasi ya utendaji ili kuharakisha maendeleo.

Aidha aliongeza kuwa maombi hayo yatasaidia kudumisha amani, umoja na mshikamano wa wananchi wote na kuongeza msukumo wa utendaji kwa kila kiongozi aliyepewa dhamana na Mheshimiwa Rais ili kutekeleza kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu kwa vitendo

No comments: